Shalom watu wa Mungu. Namshukuru Mungu kwa kunifikisha siku ya leo. Siyo kwamba nimetenda mema. Lah, ila ni mapenzi yake Mungu Baba wa Mbinguni amenipigania. Tunaungana katika mfululizo wetu wa kulisoma neno la Mungu kwa njia ya maandishi. Somo hili limefundishwa na Mtume Joshua Kachali.
Somo letu la leo kama lilivyojitanguliza hapo juu, leo tutakuwa tunajifunza kuhusu EFATHA.
Wengi watajiuliza - ‘efatha’ ni kitu gani? na kinahusiana na nini? Kinafanya kazi gani? Maswali yapo mengi lakini majibu yote yatapatikana hapa.
EFATHA maana yake nini? Efatha maana yake FUNGUKA. Hili jibu linajidhihirisha katika kile kitabu cha Marko ile sura ya 7:34-35 “akatazama juu mbinguni, akaugua, akamwambia, Efatha, maana yake, funguka. Mara masikio yake yakafunguka, kifungo cha ulimi wake kikalegea, akasema vizuri”. Hivyo kwa kuanza na huo mstari tunapata picha nzuri ya maana ya Efatha. Kwenye kile kitabu cha Luka 13:14-21 tunaona Yesu alivyomfungua yule mwanamke aliyekuwa amepindiana kwa miaka kumi na minne na akamwambia, “mama, umefunguliwa katika udhaifu wako. Akaweka mikono yake juu yake, naye akanyooka mara hiyo hiyo, akamtukuza Mungu.” Pia kwenye kile kita cha Zaburi 42:1-2 inasema, “Kama ayala aioneavyo shauku mito ya maji. Vivyo hivyo nafsi yangu nakuonea shauku.” Nafsi yangu inamwonea kiu MUNGU. Mungu aliye hai, lini nitakapokuja nionekane mbele za Mungu?.
Mtu wa Mungu, tukiangalia pia kwenye kitabu cha Mathayo 8:2 mwenye ukoma anatakaswa na kupona kabisa. Pia ile 1Wakorintho 14:1 Ufuateni upendo, na kutaka sana karama za rohoni, lakini zaidi mpate kuhutubu.
Kama tulivyoona, maana ya Efatha ambayo ni kufunguliwa, hapa tunaangalia kufunguliwa kiroho, kimwili. Kwanini tuanze kuangalia hizo sehemu mbili? Shetani anapotaka kukushambulia ana sehemu zake anazo anza nazo. Anaanza kuharibu ndani kwenye moyo halafu anamalizia mwili. Ndipo kunakuwa na vifungo vya nafsi vinavyompelekea mtu kutokuwa na maamuzi sahihi ya maisha yake kwa jambo lolote. Ndipo hapo mtu anahitajika kufunguliwa.
Unafunguliwaje? Ili ufunguliwe unatakiwa ufanye maamuzi ambayo yanatoka moyoni, akilini mwako na kusudio la maamuzi yako. Katika kitabu cha Isaya 1:19 “Kama mkikubali na kutii mtakula mema ya nchi;” Watu wamekuwa wakisubiri mpaka shetani awashambulie vya kutosha ndiyo wanageuka upande wa pili wa kukubali kufunguliwa. Hiyo inajidhihirisha katika kitabu cha Luka 15:17 kijana aliyeomba sehemu ya mali inayomwangukia baba alimpa kile alicho kihitaji. Mwanae alipokwisha kutumia zote taabu na njaa vilimpata, ikiwemo njaa kuu iliyoingia nchi ile. Alipozingatia moyoni mwake, alisema, ni watumishi wangapi wa baba yangu wanaokula chakula na kusaza, na mimi hapa nakufa kwa njaa?. Akachukua maamuzi ya kurudi kwa baba yake, baba akampokea mwanae na kumrudisha katika himaya yake.
Hata hivyo Mtumishi wa Mungu, Mtume Kachali, alisisitiza kwa watu wa Mungu kuwa na macho ya rohoni yatakayokufanya uone mambo yaliyokuzunguka na historia yake. Katika kitabu cha Yeremia 1:10-11 anasema “Angalia, nimekuweka leo juu ya mataifa na juu ya falme, ili kung’oa na kubomoa, na kuharibu, na kuangamiza; ili kujenga na kupanda. Tena neno la BWANA likanijia, kusema, Yeremia, waona nini? Nikasema, naona ufito wa mlozi.” Angalia ni jinsi gani Mungu anavyotupenda mpaka inafika mahali anakupandisha na kukuweka sehemu ya juu ya mataifa na falme ili uifanye kazi ipasavyo. Unaifanyaje kazi ya Mungu? Ndipo hapo unapotakiwa kuwa na macho ya rohoni ili kuyaona mambo yaliyokuzunguka na historia yake ndipo upambane nayo huku hayo yote yanafanyika kwa uwezo wa Mungu na Roho Mtakatifu.Mhariri: Phine Msambi, 0719317471.
No comments:
Post a Comment